Aki na Ukwa ni marafiki wawili wanaokonga nyoyo za watazamaji wa filamu nchini na Nigeria na Afrika kwa ujumla. Wawili hawa wana sifa ya ufupi huku pia watu wengi wamekuwa wakidhania ni ndugu au mapacha. Kwa mujibu wa Aki, waigizaji hao hawana undugu wao ni marafiki wazuri sana.
Marafiki hawa wamekuwa wakiishi pamoja kwa muda mrefu ingawa siku za hivi karibuni wameoneka kila mmoja akiishi kwenye makazi yake, kitu ambacho watu wengi walitafsiri kuwa huenda wametengana na kwamba inawezekana kuna ugomvi kati yao.
Kutokana na uvumi huo, Aki alijitokeza na kuzungumza na gazeti la Tribune kutoa maelezo ya kinachoendelea;
Aki ambaye jina lake halisi ni Chinudu Ikedieze anasema:
Hakuna ugomvi kati yetu suala ni kwamba sehemu tuliyokuwa tunaishi mwenye nyumba aliichukua hivyo ikatubidi tutoke. Ukweli ni kwamba hatuwezi kuishi pamoja maisha yetu yote.
Sisi ni watu wazima sasa na siku moja tunaweza kuwa na familia. Sisi sio mapacha, mimi natokea jimbo la ABIA na yeye anatokea Jimbo la IMO, ni kwamba sisi ni marafiki wazuri. Si vibaya kila mtu akienda upande wake ingawa hatukai mbali.”
Alipoulizwa kwamba umaarufu wake ulikuja baada ya kukutana na Pawpaw (Ukwa) akajibu:
Haikuwa hivyo, nimeanza kuigiza tangia mwaka 1998 wakati huo bado nasoma chuo kikuu na nikaweza kufanya kazi miaka ya 1999 na 2000. Kwahiyo nimekuwepo kabla ya Ukwa ambaye alianza kuigiza mwaka 2001 na hakuwa maarufu. Kwa muujiza wa Mungu tukajikuta pamoja na kufanya filamu ambayo tulishirikishwa na ambayo ikatupa utofauti mkubwa kwa sababu ya kimo chetu.
Ninaamini kwamba sisi sio watu pekee wafupi ila ni sanaa iliyopo ndani yetu ambayo muunganiko wake ukaipa sanaa ya filamu sura tofauti. Kumbuka hatukuanza kwa kuchekesha ingawa nilipokuwa shule ya sekondari rafiki zangu walinijua kwa uchekeshaji.
Kila jambo lililotokea maishani kwangu ni kwa sababu, na ninaamini watu wanatakiwa kujua historia yangu na maisha yangu nje ya uigizaji. Ninachoweza kusema kuja kwetu pamoja na Ukwa kulileta hamasa katika filamu za uchekeshaji.”
Kuhusu namna alivyoanza kuigiza, muigizaji huyo alisema:
Nimesoma taaluma ya mambo ya habari katika chuo kimoja huko Enugu (taasisi ya Uongozi na teknolojia). Ninakumbuka nikiwa sekondari nilikuwa kwenye kikundi cha uigizaji na vile vile nilikuwa naigiza kanisani. Ninaweza kusema hayo yote yaliijenga taaluma yangu ya uigizaji ingawa nilikuwa sijioni kama mwigizaji.
Mwaka 2004 niliweza kuhudhuria tamasha la filamu New York Marekani kwa wiki nane mfululizo, elimu ndogo niliyoipata huko ilinisaidia , ingawa kuna changamoto nyingi. Mara nyingi kukatishwa tamaa hasa tunapoenda kwenye kuchaguliwa ilikuwa kazi sana lakini sikukata tamaa mwishowe nikaweza kufanikiwa.”
Aki na mke wake
Vile vile aliulizwa kama watu walishaweza kumchukulia kama mtoto na kusema: Wote ni binadamu kila mtu akiniona kwa mara ya kwanza anafikiri ni mtoto na nikiongea fikra inabadilika na kuelewa kuwa mimi sio mtoto kama wanavyodhani. Sikujiumba mwenyewe na siwezi kujibadilisha na wala hakuna kitu ninaweza kufanya kuongeza urefu. Nimegundua ninaishi kwenye ulimwengu ambao watu walichukulia mambo wanavyodhani, hivyo watu wazima wanaweza kukutana nami na wakafanya vitu vya ajabu, wengine hunidhihaki na wengine kunicheka. Watu wengi wanashindwa kuelewa Aki wanayemwona kwenye televisheni au filamu ni tofauti sana na Chinedu Ikedieze.”
Alipoulizwa kuhusu ndoa kama imeondoa yeye kufurahia maisha alisema, maisha ya ukapera ni tofauti sana na ndoa. Kwenye ndoa unahitaji kumheshimu mwenza wako na unatakiwa kufanya mambo kulingana na mahusiano yenu hivyo kuna baadhi ya vitu itakulazimu kuviangalia kwa upya. Alisema pia anafurahia ndoa yake na anamshukuru Mungu kwa hilo ingawa anasema ni majukumu mapya tofauti na unapokuwa hujaoa.
0 comments:
Post a Comment