Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevitaka vyama vyote vya siasa
vinavyoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015, kuhakikisha vinafuata na
kuheshimu ratiba ya uchaguzi waliyojiwekea.
Katika taarifa kwa njia ya video iliyotumwa kwa vyombo vya habari,
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Kailima Ramadhani amesema kuwa
vyama vyote vilishiriki katika kuandaa ratiba hiyo na kuwa viliiridhia
hivyo hawana budi kuhakikisha wanaifuata.
“Tulikaa na vyama, mimi sikuamua hii ratiba, wao walipendekeza na
wakakubaliana na wakatoa ratiba hii, cha kwanza kabisa vyama vya siasa
wazingatie waliyoyaweka humu,” alisema Kailima.
Aliongeza kuwa utaratibu huo upo kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Uchaguzi ya 2015 na kuwa wakikiuka, sheria itawakamata.
“Kwenye maadili (Sheria ya Maadili ya Uchaguzi 2015) kuna eneo ambalo
vyama vya siasa na wagombea wanakubaliana kuzingatia muda wa kuanza
kampeni na muda wa kumaliza kampeni,” alisema.
Aliongeza kwa chama au wanasiasa watakaokiuka wataitwa kwenye kamati ya
maadili na kuhojiwa na wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria.
Agizo hilo la NEC linakuja siku chache baada ya CCM kuzindua kampeni zao
siku ya Jumapili katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam
ambapo shughuli hiyo ya uzinduzi ilihitimishwa majira ya saa 12.34
jioni, ikiwa ni nusu saa zaidi ya muda unaotakiwa kisheria.
0 comments:
Post a Comment