SIKU SABA ZATOLEWA KUJISALIMISHA WAHAMIAJI WALIOJIANDIKISHA BVR

Leave a Comment

 Tume  ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imetoa siku saba kwa wahamiaji waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kupitia mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR), 

kujisalimisha kabla ya kuchukuliwa hatua kali za kisheria.   Aidha, tume hiyo imesema zaidi ya watu 50,000  wamejiandikisha zaidi ya mara mbili na kuwataka kupeleka kadi zao katika tume hiyo mara moja na kwamba taarifa zao zimekwisha wasilishwa kwa  Jeshi la Polisi kufanyiwa uchunguzi kwa ajili ya hatua nyingine zaidi.   Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara ya kutembelea kituo cha kuchakata taarifa za wananchi 


waliojiandikisha katika daftari hilo jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Nec, Kailima Kombwey (pichani), alisema watu milioni 24.2  wamejiandikisha katika daftari hilo.  
 Alisema kati yao wapo waliofanya makosa mbalimbali wakati wa kujiandikisha na kwamba idadi hiyo inaweza kupungua baada ya kumalizika kwa uhakiki unaofanyika hivi sasa na kumalizika Septemba  15, mwaka huu.  
 Alitaja baadhi ya makosa yaliyojitokeza katika uandikishaji kuwa ni baadhi ya watu kujiandikisha pasipokutimiza umri wa kupiga kura, kujiandikisha mara nyingi na wengine wakiwa siyo raia.   Kuhusiana na idadi kamili ya wahamiaji waliojiandikisha katika daftari hilo, Kombwey alisema taarifa  itatolewa  hivi karibuni kwa vyombo vya habari. 
  Alisema kwa mfumo wa uandikishaji uliotumika mwaka huu, isingekuwa rahisi mtu kujiandikisha zaidi ya mara moja na asijulikane na kwamba tayari watu 12 wamefungwa  kutokana na kujiandikisha zaidi ya mara moja.   “Sheria inasema kwamba  yeyote anayebainika na kosa hilo kifungo chake ni miaka miwili na kwa mujibu wa sheria, mpiga kura akishafungwa zaidi ya miezi sita anakuwa siyo mpiga kura tena’” alisema.   Mbali na hilo, Kombwey pia alisema namna mfumo huo ulivyo hakuna uwezekano wa kuiba kura hivyo hakuna ulazima wa watu kukesha vituoni kulinda kura.  
  Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Benedict Wakulyambe,  ambaye alikabidhiwa ripoti ya wananchi waliojiandikisha zaidi ya mara mbili, alisema wamepokea taarifa hiyo na wataifanyia uchunguzi kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria.   Kuhusiana na maandalizi ya vifaa kwa  watu wenye ulemvu kwa ajili ya ushiriki wao kwenye kupiga kura, alisema tayari wameipa kazi kamati yao kuangalia vitu muhumu vinavyohitajika ili kufanyia kazi.

CHANZO:SOFIE MBEYU BLOG
Next PostNewer Post Previous PostOlder Post Home

0 comments:

Post a Comment