Hatimaye, Dkt.
John Magufuli ameapishwa rasmi na kuwa Rais wa serikali ya awamu ya Tano
ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania akihitimisha rasmi uongozi wa
serikali ya awamu ya nne iliyoongozwa na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.
Rais
Magufuli na makamu wake Bi. Samia Suluhu wamekula kiapo leo katika
sherehe zilizofanyika katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam mbele
ya viongozi wa nchi mbalimbali pamoja na viongozi wa chama, serikali na
viongozi wa dini ambazo zilinogeshwa zaidi na gwaride la Jeshi la
Wananchi.
Dkt. Magufuli
ameapishwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Othman
Chande na kupigiwa mizinga 21 ya heshima baada ya kukabidhiwa kijiti cha
uongozi na rais wa serikali ya awamu ya nne, Jakaya Kikwete.
Katika Jukwaa la
Kiapo, walikuwepo Jaji Mkuu, Othman Chande, Katibu Mkuu Balozi Ombeni
Sefue pamoja na Spika wa Bunge la 10, Bi. Anne Makinda na Mwanasheria
Mkuu wa Serikali.
Wengine
waliokuwa katika jukwaa la Kiapo ni pamoja na Rais wa serikali ya awamu
ya nne, Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais wa serikali ya awamu ya nne,
Dkt. Gharib Ali Bilal, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt.
Ali Shein.
Rais
wa awamu ya nne, alipigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride maalum
la jeshi la Wananchi kama ishara ya kumuaga kwa heshima na kuteremsha
bendera yake, kabla hajakabidhi madaraka kwa rais mpya Dkt. Magufuli.
Pia,
viongozi wa dini za aina Tatu walihusika katika kuunda jopo la kiapo na
kutoa sala zao kuliombea Taifa na Rais Mpya, Dkt. John Magufuli.
Marais
wa nchi mbalimbali waliohudhuria ni pamoja na Paul Kagame (Rwanda),
Jacob Zuma (Afrika Kusini), Robert Mugabe (Zimbabwe), Uhuru Kenyatta
(Kenya), Yoel Museven (Uganda), Rais wa Msumbiji pamoja na mawaziri wa
nchi mbalimbali.
Sherehe
hizo zilihudhuriwa na maelfu ya wananchi na kupata baraka ya mvua
wakati wote lakini wananchi hao waliendelea kufuatilia tukio hilo la
kihistoria.
0 comments:
Post a Comment