Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akiongea na waandishi wa habari.
Mkutano na waandishi wa Habari Ukiendelea
SERIKALI imeazimia kumaliza
migogoro yote ambayo ipo kwa wananchi ambapo Wizara ya maliasili na utalii
imeanza kuihesabu ili itatuliwe mapema iwezekanavyo ikiwa ni sehemu ya
utekelezaji wa Ilani ya Chama cha mapinduzi(CCM).
Hayo yalibainishwa na, Waziri
wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alipokuwa akizungumza na vyombo vya
habari baada ya kumaliza ziara yake wilayani Mbarali, ambapo alisema Serikali
imeona ianze upya kufuatilia suala hilo ikiwa ni pamoja na kutatua mgogoro
uliopo.
Waziri Nyalandu alilazimika
kufanya ziara Wilayani Mbarali kufuatia kuwepo kwa mgogoro wa wananchi wa
vijiji 21 kugomea kupisha hifadhi ya Ruaha.
Waziri Nyalandu alisema uamuzi
wa kuvihamisha vijiji hivyo ili kupanua hifadhi ya Ruaha ulitokana na tangazo
la Rais (GN28) la kuifanya eneo la Ihefu na vijiji vinavyoizunguka kuwa sehemu
ya hifadhi.
Alisema mgogoro huo ulianza
mwaka 2009/2010 baina ya Usangu game reserve na bonde la Ihefu kwenda Ruaha
ambapo wakazi wa maeneo hayo ambao walipangwa kuhama walitengewa fidia shilingi
Bilion 4 na baadaye kuongezwa Bilion 3 na kuwalipa fidia jumla ya Bilion 7.
Alisema baada ya hapo mgogoro
ulitokea kwa baadhi ya wananchi kudai kulipwa tofauti na makadirio, wengine
kudhurumiwa kabisa hivyo Serikali imeona
wananchi hao wasiondoke kwanza hadi madai yao yahakikiwe kwanza ambapo madai
yote yanatarajiwa kuanza kulipwa Julai 1, mwaka huu.
Aliongeza kuwa mgogoro huo
umetokana na tangazo la serikali kuandaliwa tofauti na matakwa ya wananchi, pia
maeneo yalioyoagizwa yakawa tofauti na maeneo yaliyoorodheshwa ambapo maeneo ya awali hayakuguswa kabisa.
Waziri Nyalandu alisema
kutokana na hali hiyo, wananchi hao hawataondolewa katika maeneo yao bali timu
mbili zimeundwa ili kuchunguza sakata hilo.
Alisema timu ya kwanza
itafuatilia madai yote kisha watayapeleka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambaye
atayawasilisha wizarani kwa ajili ya utekelezaji.
Alisema timu ya pili itakuwa ya
wataalamu wa Ikolojia ambao wataangalia mfumo wote wa ekolojia na maji na namna
ya kutatua mgogoro ili wananchi wawe sehemu ya hifadhi pamoja na kuangalia
namna maji yasiharibu mto Ruaha Mkuu.
Aidha alitoa wito kwa Wananchi
kuacha kuingiza mifugo yao ndani ya hifadhi ya Ruaha mkuu bali wanapaswa nao
kuwa sehemu ya uhifadhi.
0 comments:
Post a Comment