Mwanasiasa
mkongwe na kada wa CCM aliyepata kushika nyadhifa mbalimbali ikiwa ni
pamoja na uwaziri, Mzee Hassan Nassor Moyo amefukuzwa uanachama wa chama
hicho ambacho yeye ni mmoja wa waasisi wake, akiwa mwanachama namba 7.
Mzee
Moyo (81) ni miongoni mwa viongozi waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya
mwaka 1964, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar pia wa mwaka huo na mara
tu baada ya Muungano, aliteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Kufukuzwa
kwake kumetajwa kumetokana na kwenda kinyume na maadili ya chama pamoja
na matamshi yasiyokubaliana na sera za chama hicho.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa CCM mkoa wa Magharibi,
Unguja, Aziza Iddi Mapuri, matamshi mbalimbali ya Moyo aliyokuwa
akiyatoa katika mikutano ya hadhara inayofanywa na Chama cha Wananchi
(CUF) inaonesha kwamba amekisaliti chama akiwa mzee wa kupigiwa mfano
katika CCM.
Katika
taarifa hiyo, imetoa mfano kuwa Aprili 30, 2014 katika mkutano wa CUF
uliofanyika Kibandamaiti ambapo Katibu wa CUF, Seif Sharif Hamad
alimsimamisha Mzee Moyo ambaye alisema serikali tatu ndiyo msimamo wa
Wazanzibari wote.
Aidha,
katika mkutano uliofanyika Tibirinzi huko Pemba Februari 9, 2014 Mzee
Moyo alijitambulisha kuwa ni mwenyekiti wa maridhiano kutoka CCM ilhali
si kweli, kwani Chama cha Mapinduzi hakimtambui kiongozi huyo.
Katika
taarifa hiyo imesema CCM baada ya kutafakari kwa kina imebaini kiongozi
huyo amekuwa akiongoza upotoshaji wa hali ya juu na hafai kuendelea
kuwa mwanachama wa chama hicho tawala nchini.
Taarifa
hiyo iliongeza kuwa, Mzee Moyo wakati akihutubia kongamano la CUF hapo
katika ukumbi wa taasisi ya Kiswahili na lugha za kigeni, alibeza
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kusema kwamba mkataba wa Muungano
wa Aprili 22 haujulikani uliopo na wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba
walikuwa hawajui wanachokifanya.
“Kutokana
na matukio yote hayo na matamko anayoyatoa Mzee Moyo amepoteza sifa za
kuwa mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi ambaye ni mfano wa kutegemewa wa
wazee na vijana,” alisema.
Akizungumza
na mpekuzi kwa njia ya simu kutoka Tanga, Mzee Moyo alisema hajutii
uamuzi huo kwa sababu yeye hakuzaliwa kuwa mwanachama wa Chama Cha
Mapinduzi daima.
“Mimi
sijutii kufukuzwa katika Chama Cha Mapinduzi kwa sababu sikuzaliwa kuwa
mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi milele......natofautiana na CCM
katika mambo mbali mbali ikiwemo suala la muundo wa muungano,’’ alisema.
Katika
siku za hivi karibuni Mzee Moyo katika majukwaa ya CUF amekuwa akitamka
bayana kwamba muungano wa serikali mbili umepitwa na wakati na Zanzibar
ipo haja ya kuwa na mamlaka kamili.
Mbali
ya uwaziri wa Katiba na Sheria katika Serikali ya awamu ya kwanza,
nyadhifa nyingine alizotumikia Mzee Moyo katika serikali ya Muungano ni
pamoja na mbunge kwa muda mrefu na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Kwa
upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ameshika nyadhifa
mbalimbali tangu mwaka 1964 na kufanya kazi kwa karibu sana na Rais wa
Kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume kwa kuongoza Wizara ya
Kilimo kwa muda mrefu akifanya kazi kubwa ya kutekeleza ilani ya ASP ya
kugawa ardhi kwa wananchi wote.
Ni
kiongozi wa mwanzo kuwa mwanachama wa CCM ilipozaliwa mwaka 1977 baada
ya TANU kuungana na ASP ambapo katika sherehe zilizofanyika katika
Uwanja wa Amaan, Zanzibar, alikabidhiwa kadi namba 7.
Akizungumzia
suala hilo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye
alisema CCM mkoa wa Magharibi ina uwezo wa kumvua uanachama, hivyo
kilichofanyika kwa mujibu wa Katiba ya CCM ni sahihi.
Alifafanua
kuwa, kwa wanachama wa kawaida, hatua za kinidhamu zinaweza kuchukuliwa
katika ngazi za chini, bali hali ni tofauti kwa viongozi akitolea mfano
diwani, mbunge au mwakilishi ambao maamuzi ya kuwachukulia hatua za
kinidhamu yanapaswa kufanywa na vikao vya juu.
“Kwa
hiyo ndugu yangu, Halmashauri ya chama ya mkoa ina mamlaka ya kumvua
uanachama mwanachama wake wa kawaida, hivyo kilichofanyika kwa Mzee Moyo
ni sahihi kwa mujibu wa Katiba…kitakachokuja kwetu ni taarifa.
“Lakini
mengineyo, kama kwanini amechukuliwa hatua… watu wa mkoa wa Magharibi
wenyewe ndio wanaweza kueleza zaidi, sisi ni watu wa kupokea taarifa kwa
kuwa Katiba inawapa nguvu ya kufanya maamuzi ya kinidhamu,” alisema Nnauye.
0 comments:
Post a Comment